SIKU NIKIFANIKIWA
Siku nikifanikiwa, swali hili nitatiza
Kweli nitashukuriwa, na watu wasojiweza
Yatima walofiliwa, nitawapa mwangaza
Au taharibikiwa, kwa kuanza kujikweza
Watu nitawaibia, nifanikiwe kwa shari
Dhulma tawafanyia, kwa jeuri na kiburi
Uchawi nitatumia, urozi tangu dahari
Freemason taingia, nikawe hata kafiri
Au nitashughulika, fanikiwe kwa halali
Maharage taridhika, mchunga huku ugali
Ninazoa takataka, kazi yangu ni dhalili
Koradhi kusulubika, kipato kiwe halali
Nitawapa sikitiko, ndugu pia Marafiki
Tulogombea makoko, kipindi nanuka dhiki
Kutokumbuka miiko, kuwaona watubaki
Mbekenyera Kirinjiko, tulisoma kwa hilaki
Nitaheshimu wazazi, au nitawadharau
Nitakumbuka malezi, au nitayasahau
Nitamfata Mwenyezi, diniye chake kirau
Nitakuwa sijiwezi, kwa anasa na vidau
Nitafanya ihsani, au tatenda machafu
Nitakuwa kama nani, lingana wake wasifu
Nami hapa duniani, nitakuwa maarufu
Maswali mengi kichwani, fikira zangu kifipo
Tamati nimefikia, ila jibu sijatoa
Kazi ninawapatia, Islam lobakia
Mdabiri na kujua, kisha mtaniambia
Tahadhari ninatoa, nafsi kujitambua
Chanzo Annur
0 maoni:
Chapisha Maoni