1.0
Historia ya Sheikh Kaluta Amri Abedi
Sheikh Kaluta Amri Abedi alizaliwa Ujiji
Kigoma mnamo mwaka 1924 Baba yake Kaluta Amri Abedi aliitwa Abedi bin Kaluta.
Kaluta Amri Abedi Alikuwa ni mtoto wa pili wa kiume katika familia ya watoto
kumi. Sheikh Kaluta Amri Abedi alipofika umri wa miaka 6 hivi alianza masomo ya
Kurani mwaka 1930. Baada ya miaka mitatu ya masomo ya kurani aliingia katika shule ya masomo ya Kizungu. Baada ya kumaliza
elimu ya awali mwaka 1937 alijiunga na Shule ya Sekondari Tabora.Baada ya
masomo yake ya sekondari Sheikh Kaluta Amri Abed alikwenda kusomea ukarani wa
posta Dar-es-salaam 1942—1943 .Kaluta Amri Abed alikwenda kusoma elimu ya dini
Rabwah Pakistan ambako aliweza kufaulu vizuri na kuweza kutunukiwa shahada ya
elimu ya dini (Teolojia).
Sheikh.Kaluta
Amri Abedi alioa mke wake wa kwanza 1941 ambaye aliitwa Zamda bint Sudi ambaye
alibahatika kuwa na mtoto mmoja aliye itwa Radhia kabla ya kumtaliki kutokana
na upinzani mkubwa uliotokana na mgogoro wa tofauti za kidhehebu yaani Kaluta
alipo hamia madhehebu la Ahamadiyya tofauti na mke ambaye alitoka katika
familia yenye imani ya madhehebu ya sunni. Sheikh Kaluta Amri Abedi alioa mke
mwingine mwaka 1956 ambaye aliitwa Amina bint Hamisi Mlenzi ambaye alibahatika
kuzaa naye watoto sita na kufanya jumla
ya watoto saba
Sheikh
Kaluta katika maisha yake amekuwa mtumishi wa serikali kwa nyadhifa
mbalimbali,kama: aliwahi kuwa Mbunge wa kigoma, aliwahi kuwa meya wa kwanza
mwafrika wa jiji la kwanza Dar-es-salaam, aliwahi kuwa mkuu wa mkoa jimbo la Magharibi,aliwahi
kuwa waziri wa sheria,mpaka mauti yanamkuta alikuwa waziri wa maendeleo na
utamaduni.
Katika
dini Sheikh Kaluta alikuwa Sheikh na mbashiri
katika imani ya kiislam ya Ahamadiyya
alijishughulisha na kueneza dini
pamoja na kutafsiri kurani katika lugha
ya Kiswahili na lugha za kizungu.
Sheikh
Kaluta Amri Abedi alikuwa na kipaji cha usanii. Kipaji hiki cha usanii kilianza
kuonekana alipofika umri wa miaka 13, aliweza kutunga na kuimba mashairi kwa sauti nzuri na pia aliweza kudhibiti kanuni za
mizani. Aliweza kusoma mashairi ya lugha ya Kiingereza, Kiurdu, Kiarabu na
kiajemi.
2.0 Mchango wa Kaluta Amri
Abedi kwenye lugha ya kiswahili
Katika maandishi ya Mathias Eugen Mnyampala yanayotaja
historia ya maisha ya:
Sheikh Kaluta Amri Abedi, Mwandishi Mathias Eugen
Mnyampala amemtaja Kaluta kama mtu hodari wa kutumia Lugha ya Kiswahili katika
fani ya kuimba Tajuwidi, Mashairi na Tenzi kwa mahadhi ya namna mbalimbaali za Maghani. Hivyo Mnyampala anaweka bayana mchango mkubwa
wa Sheikh Kaluta Amri Abedi kwenye Lugha ya Kiswahili kama ifuatavyo:
2.1 Kaluta Amri Abedi akiwa
na umri wa miaka sita
Kaluta Amri
Abedi alionyesha dhamira ya kupenda Lugha ya Kiswahili, alianza kupigania
matumizi ya Lugha ya Kiswahili tangu akiwa na umri mdogo kati ya miaka sita,
ambapo akiwa mwanafunzi wa masomo ya Kurani alionyesha kutoridhika kujifunza
Kurani kwa Lugha ya Kiarabu tu hata akadiriki kumuuliza mwalimu wake “Kwa
nini tunasoma kama kasuku hatuelewi yaliyomo katika aya za kurani tukufu?
Kwa nini kurani haitafisiriwi katika Lugha ya Kiswahili.” Hata waalimu wake walipomjibu juu ya maneno
ya Kiarabu kuonyesha ukamilifu wa aya na madai ya Masheikh wake kwamba kurani
ikitafsiriwa ingeharibiwa maana yake tofauti na zilivyoteremshwa na Mwenyezi
Mungu, Kaluta Amri Abedi hakuridhika na majibu hayo aliendeleza jitihada za kudai
matumizi ya Lugha ya Kiswahili zaidi kuliko lugha zingine. Mnyampala (Uk. 10)
2.2 Kaluta Amri Abedi kama mshairi
Sheikh Kaluta Amri Abedi alitumia kipaji
chake cha kuimba na kughani mashairi na tenzi kuenzi matumizi ya Lugha ya
Kiswahili akizidisha maneno yenye utamu wa lugha ya Kiswahili, nahau za lugha
ya kiswahili . Hali amabayo ilifanya
kuwa motisha kubwa kwa wasomaji wa mashairi yake kuijua lugha na kuithamini kwa
utukufu wake. Sheikh Kaluta Amri Abedi alitumia kalamu kuweka mchango wake
katika kukuza lugha ya kiswahili, aliandika maandishi yanayofafanua kanuni za
utungaji wa mashairi ya kiswahili,katika kitabu chake alichokiita SHERIA ZA KUTUNGA MASHAIRI NA DIWANI YA AMRI
(1953) – Katika uandishi wake alihamasisha lugha ya kiswahili Tanzania na
Afrika Mashariki kwa umahiri wake:Kaluta aliwahi kutunga mashairi mbalimbali
kwa lugha ya kiswahili ambapo hata alipo andika kitabu cha mashairi chenye
kueleza kanuni za kutunga mashairi washairi wengiwlikipokea kwashangwe kubwa na
kumsifia Rejea Almasi ya Afrika (Uk
81) ” anaeleza hiki ni kitabu ambacho
kimesadia sana kwa wale wanao taka kujifunza utunzi wa mashairi. Ni kitabu
ambacho kinatumika mashuleni na hakuna mshairi wa sasa aliyeandika juu ya
ushairi katika karne ya ishirini ambaye hakulazimika kumnukuu”
Kaluta akiwa na umri wa miaka 13 tu
alipofiwa na baba yake aliandika ushairi wa kumwombolezea Rejerea katika Almasi ya Afrika (Uk 13-14):
Mola mrehemu baba, babaaliyenizaa,
Mola ni wewe Tawaba, mghofiri dhambi pia,
Peponi mpe maaba,na vyeo mzidishia,
Dua nitakabalia, Mola mghofiri baba,
Baba mwingi wa huruma kwa wema alinilea,
Akanitia kusoma,dini na dunia pia,
Akanifunza ya wema,ya akhera na dunia,
Dua nitakabalia Mola mghofiri baba
Baba nina
mkumbuka, vile nilivyo mjua
Mkarimu hana shaka,mwenye hadhi na sitawa,
Ni mtu alotukuka,vyeo akavipandia,
Dua nitakabalia,Mola mghofiri baba
Huu ni mfano tu wa kazi ya ushairi inayoweza
kuonyesha uwezo wake katika fani ya uga wa mashairi tangu akiwa mtoto mwenye
umri mdogo.
2.3 Kaluta Amri Abedi kama karii
Kaluta Amri Abedi
kwasababu ya umahiri wake katika kujishughulisha na lugha ya kiswahili
na uga wa ushairi alichaguliwa kuwa Karii wa mashairi ya kiswahili (yaani msomaji,
mkosoaji na mwelekezaji wa matumizi na maandishi ya lugha ya kiswahili); akiwa
Karii wa Ushairi” alipokuwa Tabora
aliandika makala zake kuhusu kiswahili akasema kwa kukitukuza kiswahili huku
akigusia historia yake na kukimanya kwakwe alisema: “Kwa bahati tu nilizaliwa katika mji ambao lugha inayosemwa ni kiswahili na utoto
wangu nikasoma karibu vitabu vyote vilivyopatikana na vilivyokuwa vimeandikwa
kwa lugha ya kiswahili kisha muda wote wa maisha yangu nikalazimika kukitumia
kiswahili kama chombo maalumu cha kufanyia kazi nilizoshughulika nazo za semi
na maandiko, ikatokea nikaanza kujali sana maneno na nguvu yaliyo nazo, ufasaha na jinsi ya kutoa
wazo lilete athari inayotakiwa, ikawa ninapoandika najitahidi kuchungua sana
maneno kuyachagua na kuyapima na kutwaa
yale tu niliyo fikiri yana nguvu za kutosha kuwasilisha maoni yangu. Mnyampala (Uk46)
Kaluta alikuwa msomaji wa vitabu vya kiswahili
aliweza kusoma maandishi ya waandishi wa kiswahili na alikosoa na kutoa maoni
yake ili kuhakikisha kiswahili kinatumiwa kwa usahihi wake, hivyo alitumia muda
wake kufuatilia maandishi na kuyafanyia marekebisho makosa ya lugha ya
kiswahili katika maandishi ya waandishi.
Hali hii ilitokana na upenzi wake mkubwa kwa lugha tukufu ya kiswahili.
2.4 Kaluta Amri Abedi kama mwanaharakati
Sheikh Kaluta Amri Abedi alichochea
kasi ya matumizi ya lugha ya kiswahili,
kwa madhumuni ya kutukuza lugha ya kiswahili. Mwandishi Mathias Mnyampala
amemfafanua Sheikh Kaluta Amri Abedi juu ya ushupavu wake katika kutetea Misingi
Imara ya Lugha ya Kiswahili. Anasema “Alikuwa hodari wa Mijadala kwa namna
zote, kwenye mashindano ya dini wakati akiwa yungali kiongozi wa dini,
alipambana kwa hoja na jamaa wengine katika lugha ya kiswahili kwa hoja
zilizokiuka alishinda katika mambo mbalimbali mororo ya kidunia,” Pia alishinda
malumbano yaliyotokea baina yake na Dkt Lyndon Harris kutokana na mashairi ya
Guni hasa yaliyo ndani ya kitabu cha kilicho tafsiriwa na Mwl. Julius K.
Nyerere kilicho andikwa na Shakespeare kinachoitwa Julius Kaisari .Mnyampala (Uk.
46 – 47)
Sheikh Kaluta Amri Abedi alisisitiza zaidi
lugha ya kiswahili huku akionyesha umma kwamba kiswahili ni lugha pekee
inayofaa kuwa ya Taifa na Serikali, alisisitiza kuwa lugha ya kiswahili
inazungumzwa na watu wengi zaidi kwa saababu imesheheni maneno mengi ya kibantu
na sarufi yake ni ya kibantu hata imekuwa rahisi zaidi wananchi kujua na
kujifunza kuliko lugha za kigeni.
Kwa msisitizo mkubwa Sheikh Kaluta Amri
Abedi kwa kubainisha uzuri wa lugha iliyotukuka, lugha ya kiswahili alifikia
kuandika maandishi ya kulikejeli kundi la watu wanaofanya juhuhudi za kujifunza
lugha ya Kiingereza, Kiarabu,na Kifaransa kwamba watazijua kwa kiasi tu, hata
kundi la wanaodhaniwa wana kijua kiingereza hakika yake ni kuwa hawakijui vilivyo,
wakisema wanakisema cha matata matata, wakiandika pia wanaandika cha matata
matata, na vyovyote vile ambavyo kujulikana kwalugha za kigeni kwa watu wengi
kutakuwa kuzijua lugha hizo juu juu tu Mnyampala (Uk48).
Ukweli Sheikh Kaluta Amri Abedi alikuwa na mapenzi ya dhati kwa lugha ya
kiswahili, hata kumbukumbu yake iliyosomwa kwenye mkutano tarehe 18/01/1962
yenye kichwa “HATIMA YA KISWAHILI” iliashiria jinsi Sheikh Kaluta anavyoshika
kalamu kwa makini kuweka bayana mapenzi makini kwenye lugha nzuri na makini ya
kiswahili akitia motisha kwa washairi wa lugha ya kiswahili pamoja na watumiaji
wa lugha ya kiswahili kuenzi, kutukuza na kuweka nia njema ya ari thabiti ya
kujifunza lugha iliyotukuka lugha ya kiswahili.Mnyampala
(Uk.47).
Sheikh
Kaluta Amri Abedi alitafsiri Kurani Tukufu kwa lugha ya Kiswahili Mnyampala (Uk14).
Alipokuwa Waziri wa Sheria alitafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili, hali hii
ilifanya shauku ya watu kujifunza sheria kwa lugha ya Kiswahili. Mnyampala (Uk.
60).
2.5 Kaluta Amri Abedi
kama mwenyekiti wa chama cha kiswahili Afrika mashariki
Sheikh Kaluta Amri Abedi alifunguliwa wigo mpana
wa kuitukuza lugha na uzuri wake pale alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama
cha Washairi wa Kiswahili kwa Afrika Mashariki,
katika kipindi hicho Sheikh Kaluta Amri Abedi alihamasisha matumizi ya
kiswahili akielezea lugha ya Kiswahili kuwa ni tunu waliyopewa kuwaunganisha,
katika kipindi hicho alishauri kiswahili
kutumiwa katika elimu ya awali, kati na
vyuo vikubwa. Kwahiyo mchango wa Kaluta
Amri Abedi ni mkubwa sana katika maendeleo na ukuaji wa lugha ya kiswahili na unafaa kuigwa na Watanzania na wana Afrika
Mashariki kwa upana wa mawazo yake katika kuienzi lugha yetu ya asili
Kiswahili.
2.6 Kaluta Amri Abedi akiwa
mwanasiasa
Sheikh Kaluta Amri Abed akiwa katika nyanja za
siasa alitumia uwanja wa siasa katika kufanya juhudi za kuhakikisha ustawi wa
lugha ya kiswahili katika matumiz, Kaluta akiwa waziri wa sheria alipiginia
kiswahili kitumiwe katika shughuri za bunge, na ulisisitiza kiswahili kitumiwe
katika kutafsiri sheria kuweka urahisi kwa sheria kueleweka kwa watu wote wa
Tanzania ambao Lugha ya kiswahili ni lugha rahisi na yenye kueleweka kwa
urahisi, Sheikh Bakri Abedi Kaluta Katika Almasi
ya Afrika ameelezea katika kitabu chake kuwa akiwa waziri wa utamaduni
aliendelea kupigania heshima ya kiswahili .Mara kwa mara alisisitiza juu ya
umuhimu wa kutumia kiswahili katika shule zetu kuanzia shule za msingi hadi
chuo kikuu.Sheikh Kaluta Amri Abedi kuonesha uzalendo katika lugha ya kiswahili
aloiwahi kuwaondoa watoto wake kutoka shule ya msingi Agha Khan ambayo leo
inaitwa Muhimbili, na kuwahamishia shule ya msingi ya Mnazi mmoja iliyo kuwa
ikifundisha kwa kiswahili hiyo ilitokana na alipogundua watoto wake hawawezi
kusoma vitabu vya dini vilivyo andikwa kwa kiswahili, Katika (Uk
209-210). Pia Sheikh Kaluta akiwa waziri wa Utamaduni na maendeleo ya jamii
aliwahi kuwa mmoja ya watu waliopendekeza kuanzishwa kwa Taasisi ya uchunguzi wa
kiswahili ili iwe Taasisi yenye kusimamia matumizi ya kiswahili, Kwa mchango
wake katika shughuli zake kuienzi lugha ya kiswahili Taasisi ya Ukuzaji wa
Kiswahili wliamua kumtunuku cheti cha kumbukumbu ya Jubeleiya TUKI ya miaka75
tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930-2005.
Sheikh
Kaluta Amri Abedi ametoa mchango mkubwa katika lugha ya kiswahili akiwa katika
nyazifa mbalimbali kama ilivyo oneshwa kuwa alikuwa mwanaharakati wa kiswahili,
Mshairi ambapo alitunga mashairi kwa kiswahili na kuimba lakini pia alikuwa
mwandishi wa kitabu cha kanuni za kutunga mashairi,alikuwa mwanasiasa
aliyetumia mwanvuli wa siasa kuendeleza juhudi za kuitukuza lugha ya kiswahili
na kuendelea kuipigania itumike katika shughuli za bunge na pia shule za
msingi, sekondari na hata vyuo vikuu,aliwahi kuwa karii na hata mwenyekiti wa
chama cha mashairi Afrika mashariki.Wakati wote huu Sheikh Kaluta Amri Abedi
alishadadia kiswahili kupewa kipeombele zaidi katika matumizi Tanzania na
Afrika mashariki yote.Kwa kweli Sheikh Kaluta Amri Abedi ametoa mchango mkubwa
katika kukua kwa lugha ya kiswahili anafaa kuigwa na kuenziwa na Watanzania na
Wana Afrika mashariki kwa jumla.
MAREJELEO
Abeid,
B.K.A (2010) Almasi ya Afrika- Maisha ya
Sheikh Kaluta Amri Abeid 1924 – 1964.
Ahmadiyya Printing
Press, Dar es Salaam.
Abidi,
K.A (1954) Sheria za Kutunga Mashairi na
Diwani ya Amri. East African Literature
Bureau.
1 maoni:
Naomba kuelezwa kanuni za mashairi alizoangazia
Chapisha Maoni