Matini Muhimu :
Home » » Kiswahili Marekani

Kiswahili Marekani

Imeandikwa na; Unknown mnamo, Ijumaa, 3 Januari 2014 | Ijumaa, Januari 03, 2014




SWAHILI FORUM 15 (2008): 121-133



UFUNDISHAJI WA KISWAHILI MAREKANI: MAENDELEO
                  NA CHANGAMOTO 
                         
                                     J. KIARIE WA'NJOGU


1. Utangulizi

Kiswahili ni mojawapo ya lugha za Kiafrika zinazofundishwa nchini Marekani. Lugha
zingine ni Kiyoruba, Kizulu, na Kihausa (tukitaja chache tu). Kunazo lugha zingine za
Kiafrika ambazo hufundishwa kutegemea mahitaji ya wanafunzi. Lugha hizi ni kama vile Ki-
wolof, Kitwi, Kitigrinya, Kiamharik, Kilingala na kadhalika. Lugha za Kiafrika zimekuwa
zikifundishwa Marekani kuanzia miaka ya hamsini, kupitia mswada uliopitishwa na bunge wa
Elimu ya Ulinzi wa Taifa (National Defense Education Act - NDEA) wa mwaka 1958 (Bo-
kamba 2002). Mswada huo ulipelekea kuanzishwa kwa vituo vya ufundishaji wa mambo ya
Afrika na masomo ya maeneo mengine (African and other area study centers). Kuanzishwa
kwa vituo hivi kulikuwa kama njia moja ya kujaribu kukabiliana na maenezi ya Ukomunisti.
Pia wakati huo huo, kulikuwa na msukumo kutoka kwa Waafrika-wa-Amerika (Waamerika
wa asili ya Afrika) uliosababishwa na kutofundishwa mambo yaliyohusu historia na
utamaduni wao. Msukumo huu pia ulichangia katika kuanzishwa kwa lugha za Kiafrika katika
vyuo vya elimu ya juu. Baada ya Vita Baridi kuisha na kuvunjika kwa muungano wa Sovieti,
Marekani ilihimiza lugha fulani zifundishwe kwa maslahi ya mahitaji yake ya kiuchumi na
usalama. Miongoni mwa lugha zilizofikiriwa kuwa muhimu ni Kiamharik na Kizulu (Mazrui
1997). Kiamharik kilipendelewa kwa sababu ya kuwa karibu na eneo la Arabia, lililo na uta-
jiri mwingi wa mafuta ya petroli. Lugha ya Kizulu ilipendelewa kwa sababu ya utariji wa
maadini katika Afrika ya Kusini na nafasi ya nchi hiyo katika siasa za bara la Afrika kwa
jumla.

  Kutokana na kuanzishwa kwa lugha za Kiafrika katika elimu ya juu, vyuo vinavyofundisha
lugha ya Kiswahili Marekani vimeongezaka kufikia zaidi ya hamsini. Kwa sababu ya tofauti
katika ufadhili wa lugha za Kiafrika, programu nazo hutofautiana katika raslmali au vifaa
vilivyomo vya kufundishia, ujuzi wa kufundisha, mbinu za kufundisha, na hata kukua kwa
progamu zenyewe (Folarin-Schleicher na Moshi 2000). Katika makala hii tutaelezea ufun-
dishaji wa lugha ya Kiswahili, utayarishaji wa walimu na vifaa, na matatizo yanayokumba
ufundishaji wa Kiswahili (na lugha zingine za Kiafrika kwa jumla) kama lugha ya kigeni.
Mwisho tutapendekeza njia za kusuluhisha kwa matatizo haya. 

Historia fupi ya Kiswahili Marekani

Kama tulivyotaja hapa juu, lugha za Kiafrika zilipoanzishwa Marekani hazikujisimamia (na
bado hazijajisimamia katika vyuo vingi) kama idara. Badala yake zilikuwa kama 'nyongeza'
katika idara mbalimbali kama vile Isimu, Masomo ya Waafrika-wa-Amerika (African-Ameri-
can Studies), na Idara ya Fasihi, Idara ya Fasihi-Linganish, au Idara ya Masomo ya Kimataifa.
Mwanzoni, walimu waliochukua nyadhifa za kusimamia au na kufundisha lugha hizi wali-
fanya hivyo kwa kujitolea au kama kazi ya ziada. Waaafrika wachache waliokwenda Mareka-
ni kuendelea na masomo yao katika idara mbalimbali waliweza pia kutumiwa kufundisha lu-
gha zao kwa malipo (ingawa ya chini). Malipo haya yalikuwa kwa kulipiwa karo/ada za shule
na mshahara mdogo kila mwezi kugharamia maisha na mahitaji ya shule (Sanneh na Omar
2002).

  Wizara ya mambo ya Kigeni ya Marekani ilihitaji wafanyakazi wa kuhudumu katika bara
la Afrika na kwa hivyo walichapisha vitabu vya kwanza vya kufundishia lugha za Kiafrika.
Swala ambalo lilikabili kuanzishwa na kufundishwa kwa lugha za Kiafrika Marekani lilikuwa
la kuamua ni lugha zipi (miongoni mwa zaidi ya 2500) zifundishwe. Mwaka wa 1979 walimu
wa lugha za Kiafrika na wawakilishi wa vituo vya masomo ya Kiafrika walikutana katika
Chuo Kikuu cha Jimbo la Michigan. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kutoa mwelekeo na
kipaumbele ufundishaji wa lugha za Kiafrika. Mkutano huo ulitoa orodha ya lugha za kufun-
dishwa kwa kuzingatia maswala ya ndani ya Afrika, kama vile idadi ya wasemaji na matumizi
ya lugha hizo kama lugha za pili. Orodha kamili ilikuwa na lugha ishirini na nne
zilizofikiriwa kuwa muhimu kama lugha za taifa na za kimataifa. Orodha hii ilitofautianan ki-
dogo na ile ya Wizara ya Elimu kwa sababu yao iliongozwa na maswala ya ulinzi wa taifa.

  Mwaka wa 1980 NDEA ilifutiliwa mbali na badala yake kukawa na Halmashauri ya Elimu
ya Juu (Higher Education Act). Kupitia msaada wa halmashauri hii, waratibu wa lugha za
Kiafrika huweza kukutana kila mwaka kujadiji njia za kuzipa nguvu lugha hizi. Mswada huu
ulitiliwa nguvu zaidi baada ya kuanzishwa kwa vyama vya wataalamu kama Vituo Vya Taifa
vya Lugha za Kigeni (National Foreign Language Centers-NFLC) mwaka 1987, na
Shirikisho la Walimu wa Lugha za Kiafrika (African Language Teachers' Association-ALTA)
mwaka 1988 (Sanneh na Omar 2002). Wakati huo huo, kwa mara ya kwanza, udhamini wa
Fullbright-Hays ulitolewa kwa wanafunzi wa Kihausa na Kiswahili ili kuwawezesha kushiriki
katika kujifunza lugha hizi ng'ambo wakati wa kiangazi (Group Projects Abroad-GPA).
Kufikia sasa kuna udhamini wa lugha tatu (Kiswahili, Kizulu na Kiyoruba) katika mradi huu.
Programu ya Kiswahili huwapeleka wanafunzi Tanzania, progamu ya Kiyoruba huwapeleka
wanafunzi Nigeria, na ile ya Kizulu huwapeleka wanafunzi Afrika Kusini. 

  Katika miaka ya tisini, programu za lugha za Kiafrika zilifanya warsha mbalimbali ili ku-
wazoesha walimu wa lugha husika mbinu za kufundisha na kutahini usemaji wa lugha hizo.
Mbinu hizi zilitayarishwa na kupendekezwa na Baraza la Amerika la Ufundishaji wa Luhga
za Kigeni (American Council on the Teaching of Foreign Languages-ACTF). Mapendekezo
haya yalikubaliwa na wote waliohusika na utekelezaji wake ukaanza mara moja. Kwa bahati
mbaya, utekelezaji huu haukudumu kwa sababu ya kubadilikbadilka kwa walimu wa lugha za
Kiafrika. Tatizo hili litajadiliwa hapo chini.

  Kutokana na msaada wa Chama cha Taifa cha Mashirika ya Lugha Zisizofundishwa sana
(National Council of Organizations of Less Commonly Taught languages- NCOLCTL),
ALTA iliweza kugharamia mfululizo wa pili wa warsha za kujadili mpango wa kufundisha
lugha hizi. Kuliundwa vikundi vya kushughulikia lugha tatu zilizoonekana zikifundishwa
sana. Lugha hizi zilikuwa Kiswahili, Kiyoruba na Kizulu. Baadaye, vikundi hivi vilipanuliwa
zaidi na wajibu wake kuongezwa na kuwa vikundi vya kushughulikia lugha za Afrika Kusini,
Mashariki na Magharibi (Southern, Easter, and Western Africa Language Task Forces).

  Mwaka wa 1993, Taasisi ya Kiangazi ya Ushirika wa Lugha za Kiafrika (Summer Coop-
erative Afrian language Institute-SCALI) ilifanyika kwa mara ya kwanza katika Chuo Kikuu
cha Yale. Taasisi hii iliweza kutumia rasilmali kutoka vyuo husika na kuleta pamoja wana-
funzi kutoka vyuo mbalmbali, ambao, zaidi ya kubadilishana mawazo ya utafiti wao, waliji-
funza mojawapo wa lugha za Kiafrika zilizofundishwa. Tangu wakati huo, taasisi hii hufany-
ika kila kiangazi na chuo chochote kinachoamua kuchukua jukumu la kuiandaa, hulazimika
kufanya hivyo kwa miaka miwili mfululizo, kisha huhamia katika chuo kingine. Wanafunzi
wa shahada ya pili au zaidi wanaweza kuomba msaada wa kifedha wa kushiriki katika pro-
gramu hii kutoka mfuko unaogharamiwa na Wizara ya Elimu ya Marekani kupitia programu
inayoitwa kwa kifupi FLAS (Foreign Language and Area Studies).

Sababu za Wamarekani kutaka Kujifunza Kiswahili

Vihamasishi vya lugha na masomo ya Kiafrika vinaweza kujitokeza kwa njia mbili kuu: sa-
babu za chuo-husika na sababu za wanafunzi wenyewe. Sababu za chuo ni kama vile kuweka
mahitaji ya lugha za Kigeni. Vyuo kadhaa huwahitaji wanafunzi kutosheleza mahitaji ya
lugha ya kigeni kwa kujifunza lugha nyingine zaidi ya lugha ya kwanza. Katika kiwango hiki,
lugha ya Kiswahili hushindana na lugha zingine za kigeni zinazofundishwa. Lugha hizi huto-
fautiana kutoka chuo kimoja hadi kingine. Lugha ya Kiafrika (kama Kiswahii) pia inaweza
kuwa sehemu ya shahada inayotolewa na idara/programu ya masomo ya Kiafrika. Sababu za
wanafunzi ni nyingi na hutegemea mwanafunzi mwenyewe. Baadhi ya sababu hizi ni mahitaji
ya utafiti, kumwezesha mwanafunzi kupata ufadhali, biahsara ya kimataifa, hata kumwezesha
mwanafunzi kuwasiliana na mpenzi wake (Wa_Njogu 2005). 

  Kunao pia wanafunzi ambao walijaribu kujifunza lugha zingine za Uropa bila mafanikio.
Hawa nao huja kujaribu lugha ambayo ni tofauti kabisa la lugha yao ya kwanza au na lugha
yoyote ile ambayo huwa wamejaribu kujifunza. Utafiti umeonyesha kwamba baadhi ya ujuzi
wa lugha ya kwanza unaweza kutumika katika kujifunza lugha ya pili (Odlin 1989). Kwa sa-
babu Kiswahili hutumia hati za Kirumi, wanafunzi hawahitaji kujifunza hati mpya kama
ilivyo katika madarasa ya Kichina, Kiarabu, Kikorea, Kijapani na mangineyo. Baada ya ma-
zoezi machache, wao wanaweza kutumia ujuzi wao wa lugha ya kwanza na kusoma. Ingawa
haijathibitishwa kiutafiti, kwa vile Kiswahii huandikwa jinsi kinavyosemwa au kutamkwa
inakuwa rahisi kwa mwanafunzi kukuza mbinu za kusema na kuandika kwa wakati mmoja.

  Kama inavyojitambulisha, Marekani ni nchi yenye wahamiaji kutoka nchi nyingi. Nchi za
bara la Afrika nazo hazikubakia nyuma katika swala hili la uhamiaji. Watoto wa wahamiaji
hawa huhiari kujifunza lugha ambayo wanaweza kujihusisha au kujitambulisha nayo, na kwa
minajili ya kuendeleza utamaduni wao. Wanafunzi ambao wanaweza kusema Kiswahili, hu-
himizwa kuchukua madarasa ya juu kama yale ya fasihi, lakini wale ambao wamezaliwa na
kukulia Marekani huanza na madarasa ya chini kama Wamarekani wenzao. Kwa sababu ya
uwezekano wa kupanuka kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili barani Afrika, madarasa ya
Kiswahili pia huwavutia wanafunzi kutoka bara Ashia kama vile Wachina, Wajapani, na Wa-
korea.

  Kunao wanafunzi ambao hujifunza Kiswahili kwa sababu wanatarajia kuzuru Afrika ya
Mashariki. Licha ya wale ambao wanahusika na usomi, kunao wengine ambao wana-
jishughulisha na miradi hasa ya kidini na huhitaji ufahamu wa lugha na utamaduni wa Kiswa-
hili. Mara kadha kunapatikana wanafunzi ambao ni watu waliostaafu na wanaotarajia kuzuru
Afrika kama watalii. Katika Marekani watu wa umri wa juu wanaruhusiwa kujisajilisha mada-
rasa katika vyuo vya serikali bila malipo yoyote. Kwa hivyo wakati mwingine kunapatikana
wanafunzi wazee ambao wanajitayarisha kutembelea Afrika ya Mashariki. Kwa jumla wana-
funzi ambao hujiunga na madarasa ya Kiswahili kwa malengo yao wenyewe (zaidi ya maa-
muzi ya chuo) huwa na ari zaidi ya kujifunza. Jambo hili limethibitishwa na watafiti wanao-
jishughulisha na msukumo unatokana na mwanafunzai mwenyewe na ule unaotoka nje (in-
trinsic and extrinsic motivation) (kama vile Gardner (1996)).

  Shule nyingi za msingi na sekondari nchini Marekani hazifundishi mambo ya Afrika. Kwa
hivyo mambo mengi ambayo wanafunzi wanajua kuhusu Afrika ni yale yanayotokana na
vyombo vya habari kama magezeti na televisheni. Mambo mengi huwa si ya kweli, na ha-
yalengi kuonyesha picha nzuri kuhusu Afrika. Mara nyingi huwa ni habari zinazohusu njaa,
magonjwa, vita vya kikabila, ukame na kadhalika. Madarasa ya Kiswahili hujalizia mapango
haya kwa kufundisha historia, jiografia, siasa, dini na imani mbalimbali za Afrika (miongoni
mwa mengine) zaidi ya kufundisha lugha. Pia madarasa ya Kiswahili hutoa nafasi nzuri ya
kukosoa na kurekebisha imani hizi potovu miongoni mwa baadhi ya wanafunzi.

  Baada ya uvamizi wa kigaidi wa Septemba 11, 2001 umuhimu wa lugha za kigeni
umetiliwa mkazo sana na serikali ya Marekani. Kwa sababu hiyo vyuo vinavyoweza kutoa
mafunzo ya juu kwa wanafunzi wao katika lugha za kigeni vinapata ufadhili mkubwa kutoka
serikalini. Maingilio ya serikali katika kuathiri mafunzo vyuoni hayajachukuliwa vizuri na
walimu wengi kwa sababu malengo ya serikali na ya vyuo hayalingani. Kwa kuwa sababu za
wanafunzi za kujifunza Kiswahili kama lugha ya kigeni ni nyingi na tofauti, silabsi, vifaa, na
mbinu za kufundishia nazo hulenga kutosheleza malengo hayo. Hata hivyo ufundishaji wa
Kiswahili kama lugha ya kigeni Marekani hukumbwa na matatizo tofauti. Sasa tutayaangazia
baadhi ya matatizo hayo. 



Matatizo ya Kufundisha Kiswahili kama Lugha ya Kigeni

Matatizo haya yanaweza kuchunguzwa katika vipengele tofauti kama vile: walimu, vifaa,
wanafunzi, na ufadhili.

1. Walimu

Wengi wa walimu wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni hawajachukua mafunzo ya
kazi hiyo. Wengi wao ni wanaisimu na hufundisha lugha hizi kwa sababu ya uwezo wao wa
kuzisema kama lugha ya kwanza, au kwa sababu ya ujuzi wao katika lugha hizi. Tatizo
lingine ni kwamba kazi za walimu hawa ni za muda tu, na wala si za kudumu. Kwa hivyo
muda wao mwingi huutumia kujishughulisha na mambo mengine ya utafiti wao badala ya
Kiswahili. Walimu hawa basi hutegemea sana uzoefu wao na vipawa vyao (Batibo 2003).

  Kulingana na Moshi na Schleicher (2000) chini ya asili mia 10 ya vyuo na vyuo vikuu vi-
navyofundisha lugha za Kiafrika vina walimu wa kudumu wa kufundisha lugha hizi. Ajabu ni
kwamba kati ya vyuo hivi hakuna hata kimoja chenye programu iliyoanzishwa kwa ufadhili
kutoka kwa serikali. Sababu ya tukio hili ni kwamba vyuo vilivyo na walimu wa kudumu vil-
ianzisha programu zao bila kutegemea mfuko wa serikali na kwa hivyo vilitenga fedha kwa
madhumuni ya kukuza programu zao. Hata hivyo walimu hawa huhitajika kufundisha
masomo mengine katika nyanja zao za kitaaluma kama vile isimu au fasihi. Kwa sababu
tathmini za kazi zao hutegemea sana masomo haya mengine, walimu hawa huzingatia
masomo haya zaidi ya lugha katika utafiti wao.

  Asilimia kubwa ya walimu wa Kiswahili huwa pia ni wanafunzi wa shahada za uzamili au
uzamifu. Wengi wa wanafunzi hawa huwa wanaendelea na masomo yasiyohusiana na lugha
ya Kiswahili au mbinu za ufundishaji wa lugha za kigeni. "Utaalamu" wa walimu hawa huwa
ni ule wa kuisema lugha ya Kiswahili tu. Ingawa walimu hawa hujibidiisha kufanya kazi
nzuri, huwa wanakumbwa na tatizo la kuishiwa na muda wa kujitayarisha kwa masomo yao
wenyewe na kujitayarisha kwa masomo ya kufundisha. Na kana kwamba haya si matatizo ya
kutosha, vyuo vingi haviwatambui wanafunzi hawa kama wafanyakazi wa chuo na kwa hivyo
mishahara yao huwa duni na hawawezi kujiunga na vyama vya wawakilishi wa wafanyakazi
vinavyoweza kuwatetea maslahi yao. Ingawa walimu hawa wanapewa jina la walimu-wa-
saidizi, walimu ambao huwa wanastahili kuwasaidia huwa hawaingii madarasani haya mara
nyingi (isipokuwa wakati wa ukaguzi wa kazi).

  Kunao pia walimu wengine ambao huwa na shughuli zingine mijini na hupewa kazi ya
kufundisha Kiswahili kwa malipo ya masaa hayo tu wanayofundisha. Walimu hawa huajiriwa
kwa masaa kwa sababu labda chuo hakina pesa au hakitaki kutumia pesa katika programu ya
lugha za Kiafrika, na huishia kuchukua hatua hii kwa sababu ya msukumo wa wanafunzi.
Hatua hii inaweza kushusha hadhi ya lugha na masomo ya Kiafrika kwa jumla.

Wanafunzi wanaofundishwa na walimu ambao hawakuhitimu katika masomo yao huwa ha-
wayazingatii sana masomo haya. Pia, kwa sababu ya uhaba katika ujuzi miongoni mwa
walimu wasiofuzu, kuna uwezekano wa kuishia kufundisha vitu vilivyo rahisi kwao badala ya
kuzingatia mahitaji ya wanafunzi na programu kwa jumla. 

2. Rasilmali na Vifaa

Kwa jumla kuna uhaba wa rasilmali na vifaa vya kufundishia Kiswahili kama lugha ya kigeni.
Vifaa vinavyotumiwa aghalabu huwa katika hali ya vitabu, kanda za kunasia sauti, kanda za
video, visahani vya CD, na tovuti/mtandao. Kila kifaa cha kufundishia huwa kimetengenezwa
kukidhi au kutosheleza mahitaji fulani. Kwa vile malengo ya wanafunzi wanaojisajilisha
katika madarasa ya Kiswahili ni tofauti, kuna haja ya kuwa na vifaa tofauti ili kutosheleza
mahitaji yao. Kwa mfano wanafuzi wa isimu hutaka masomo yapangwe kwa kuzingatia mi-
undo ya sarufi. Wanafunzi ambao wangetaka kuzungumza zaidi huhitaji masomo yapangwe
kwa njia ya mazungumzo ili waweze kushirikishwa sana katika mazungumzo. Kuna wana-
funzi ambao hutaka kuwa na ufahamu zaidi wa utamaduni na kwa hivyo huhitaji mambo ya
utamaduni yapenyezwa katika karibu kila somo. Vifaa vingine pia huzingatia mbinu za wana-
funzi za kujifunza. Kuna wanafunzai ambao hutaka kuyatazama mambo kijumla, na wengine
hutaka kutazama mambo kwa vipengele vyake. Mpaka sasa hakujatolewa kifaa kinachojisi-
mamia chenyewe katika kutosheleza mahitaji ya mwalimu, wanafunzi, progamu na chuo.
Vyuo vingine havina maabara ya lugha za kigeni. Walimu wengine hawana uzoefu wa ku-
tumia vifaa vya kiteknolojia na huhiari kuendelea kutegemea ubao na chaki ilhali wanafunzi
wangependelea vifaa vya kisasa kuhusishwa katika madarasa yao ya lugha.

Vitabu

Katika mwaka wa kwanza kuna vitabu kadha vinavyotumiwa kufundishia Kiswahili kama
lugha ya kigeni. Vitabu hivi ni Kiswahili:Msingi wa Kusema, Kusoma, na Kuandika cha
Thomas Hinnebusch na Sarah Mirza; Kiswahili kwa Kitenda cha Sharifa Zawawi; Tujifunze
Kiswahili cha John Mugane; Tuseme Kiswahili cha Senkoro miongoni mwa vingine. Kuna vi-
tabu vingine lakini hivyo hutumiwa kama vya ziada na marejeleo. Vitabu tulivyotaja vime-
jaribu kuwasilisha lugha na utamaduni kwa njia mwafaka kwa wanafunzi wa mwaka wa
kwanza. Vitabu hivi vimeanza kwa mambo ya kimsingi kwa kuzingatia kwamba watumizi wa
vitabu hivi hawana ufahamu wowote wa maisha katika Afrika ya Mashariki (Biersteker and
Bennett 1986). Mazungumzo, ufahamu, sarufi na mazoezi vinatosheleza mahitaji ya kiwango
hiki. Udhaifu mkubwa wa vitabu vya mwaka wa kwanza ni kuegemea sana katika sarufi.
Maoni ya mwandishi ni kwamba kwa vile waandishi wa vitabu hivi ni wanaisimu, walidhani
wanafunzi wote wa Kiswahili ni wanaisimu au wana ujuzi wa isimu au wanastahili kuwa na
ujuzi huo. Kwa mfano, kitabu cha Mugane kimejaa maelezo ya migao katika vitenzi na ma-
kubaliano ya irabu. Ingawa maelezo haya yanawafaa walimu na wanafunzi wa isimu au wana-
funzi walio na elimu ya kiisimu, kwa wanafunzi wengi hizi ni habari za kuwapoteza zaidi.
Udhaifu mwingine ni wa kutegemea michoro badala ya picha halisi. Picha halisi huonyesha
jinsi kitu kilivyo na hali ilivyo katika uhalisi wake. Michoro inaweza kufikiriwa kama maoni
ya mchoraji na ukweli wa mambo unaweza kutojitokeza katika michoro. Udhaifu huu
unaonekana sana katika kitabu cha Hinnebusch na Mirza. Kitabu cha Senkoro kimeuepuka
udhaifu huu kwa kutumia picha halisi. Hata hivyo kuna picha nyingi ambazo hazikuelezewa
zinawakilisha nini na mpangilio wa masomo unakosa mtiririko. Baadhi ya masomo magumu
yanakuja mapema mno. Katika mwaka wa pili, walimu huchukua mikondo tofauti. Katika
kiwango hiki baadhi ya walimu huwatanguliza wanafunzi wao katika usomaji wa magazeti,
vifungu vifupi au na hadithi fupi. Pia masomo mengi huwa yameegemea sana katika
utamaduni. Baadhi ya masomo ambayo hufundishwa ni familia, malezi ya watoto, majukumu
ya watu tofauti katika familia, masomo ya jadi na ya kisasa, siasa, bishara, uchumi, n.k. Hata
hivyo hakuna vitabu vilivyoandikwa kuhitimisha mahitaji katika kiwango hiki. Miongoni
mwa vitabu vinavyotumiwa ni: Tuimarishe Kiswahili Chetu na Kiswahili Lugha na
Utamaduni vya Lioba Moshi; na Masomo ya Kisasa cha Ann Biersteker. Udhaifu mkubwa wa
vitabu hivi ni ukosefu wa mazoezi ya kutosha kupima uwezo tofauti wa wanafunzi. Mengi ya
mazoezi yaliyopo ni ya ufahamu. Katika mwaka wa tatu na wa nne (wanafunzi wanapopati-
kana) walimu huchukua mikondo tofauti kutegemea mahitaji ya wanafunzi. Mkondo mkuu ni
wa kuwatanguliza fasihi pamoja na kuendelea na sarufi zaidi. Hata hivyo kumeanza kuzuka
fikra kwamba sio wanafunzi wote wanaotaka ujuzi wa kuchambua fasihi. Badala ya kuchukua
mkondo huu, mawazo ya kuhusisha taaluma nyingeinezo yameanza kusambazwa na ku-
tekelezwa katika lugha zingine za kigeni. 

Kanda za kunasia sauti, Filamu, Video, na Visahani vya CD, VCD na DVD

Matoleo ya kwanza ya Kiswahili: Msingi wa kusoma, kusema, na kuandika na Kiswahili kwa
kitendo yaliambatana na kanda za kunasia sauti. Kila somo lilikuwa na ukanda wake. Kanda
hizi hazikutoa mafunzo au mazoezi zaidi ya yale yaliyokuwa katika vitabuni vilivyohusika.
Kuna kanda zingine zilizotayarishwa kwa madhumuni ya kujifunza Kiswahili, lakini hizi
zimewalenga watalii. Kanda hizi zimetayarishwa na wafanyabiashara bila kuzingatia mbinu
za kujifunza na kufundisha lugha ya kigeni. Kanda hizi huwa ni mkusanyiko wa vifungu
vinavyofikiriwa na watayarishaji kwamba vitahitajika kwa mawasiliano ya kimsingi.

  Kuna video chache zilizotengenezwa kwa madhumuni ya kufundishia Kiswahili. Kwa
mfano: Kiswahili: Lugha na Utamaduni. Video hizi zilitayarishwa na Lioba Moshi wa chuo
kikuu cha Georgia kupitia ufadhili wa Wizara ya Elimu ya Marekani. Video hizi zimelengewa
wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili na huandamana na kitabu. Kwa jumla kuna video
nane zenye masomo ishirini na nne. Mambo mbalimbali yamehusishwa katika video hizi.
Kwa mwalimu ambaye hajui jinsi ya kutumia video kufundishia, atakuwa na kazi ngumu
kwani hakukutolowa mazoezi katika video wala katika kitabu. Video zingine ziko katika
lugha ya Kingereza, kwa mfano, The Africans: A tripple heritage za Ali Mazrui. Video hizi
huweza kutazamwa na wanafunzi hujadili katika Kiswahili.

  Kuna filamu kadhaa ambazo zinaweza kujumuishwa katika vifaa vya kufundishia. Filamu
hizi ni kama Arusi ya Mariamu, Maangamizi, Tusamehe, na Bongoland 1 na 2. Filamu za
kwanza mbili zimetumiwa kwa kiasi na walimu katiak viwango mbalimbali. Maoni ya wengi
ni kwamba filamu hizi zinaweza kutumiwa kwa wanafunzi wa mwaka wa pili na ziadi.   

  Kufikia sasa hakuna visahani vingi vya CD vya kufundishia Kiswahili. Kampuni ya
Rosetta Stone imetoa kisahani kimoja cha Kiswahili. Mafunzo na mazoezi ya kisahili hiki
yanategemea picha na sauti. Picha karibu zote zilizotumiwa zimepigwa Marekani na kwa
hivyo hazitoi uhalisi wa mambo kama yalivyo katika Afrika ya Mashariki. Michezi mingi
inayoingizwa na kuonyewha katika runinga za Afrika ya Mashariki (hasa Kenya na Tanzania)
sasa inapatikana katika DVD na VCD. Shida ni kuwa baadhi ya visahani hivi haviwezi
kuchaza moja kawa moja katika mitambo ya Marekani kawa sababu ya tofauti baina ya
mitambo.

Mtandao

Katika mtandao kuna mafunzo ya Kiswahili si haba yanayotolewa na makampuni, watu binaf-
ssi na shule. Kwa sababu ya mahimizo katika matumizi ya kompyuta, walimu wengi wa-
mejibidiisha kuweka kazi zao kwenye mtandao. Wafanya biashara nao wamechukua nafasi ya
kuweko kwa kifaa hiki kuenezea biashara zao. Matumizi ya mtandao yanaelekea kuwa na
faida kwa sababu wanafunzi wanaweza kufanya kazi zao wakati wowote na mahali popote na
kumpelekea mwalimu wao kwa barua pepe. Kwa kufanya hivyo pia inapunguza gharama ya
karatasi. Mtandao pia umewawezesha wanafunzi na wapenzi wa Kiswahili kuweza kusema na
kusikiliza habari na vipindi mbalimbali katika lugha ya Kiswahili kutoka maeneo mengi
Kiswahili kinakotangazwa kama Ujerumani, Wingereza, Ujapani, Afrika-Kusini n.k. Shida
iliyopo ni kwamba kurasa nyingi zilizoko kwenye mtandao zinahitaji kuhaririwa kwani zime-
jaa makosa hasa ya kisarufi. Hata hivyo kuna kurasa chache za mtandao ambazo zinafaa. Ku-
rasa hizi ni kama KAMUSI (ya Ann Biersteker na Martin Benjamin), KIKO (ya Liomba
Moshi na Alwiya Omar) na SALAMA (ya John Mugane) miongoni mwa zingine.

  Licha ya kuwawezesha walimu na wanafunzi kutazama maneno kutoka Kiingereza hadi
Kiswahili au kutoka Kiswahili hadi Kiinereza, KAMUSI huwa na nafasi ya mazungumzo na
viungo vya mambo mbalimbali kama habari (kutoka nchi mbalimbali-Afrika na Ulaya), na
maonyesho ya picha kutoka Afrika Mashariki. KAMUSI ina maneneo zaidi ya 50,000 na
bado haijakamilika. KIKO ina visehemu vya video. Kwa hivyo wanafunzi wanaweza kuona
vitendo vikifanyika na kusia sauti. Ukurasa huu pia unaweza kutumiwa na wanafunzi wa
Kiswahili mahali popote. Ukurasa wa SALAMA huhitaji idhini kutoka kwa mtayarishi.
Masomo ya mwaka wa kwanza na wa pili yamekamilika. Kuna picha na sauti pamoja na
kamusi katika ukurasa huu.  

3. Ufadhili 

Kama tulivyoona hapo juu, Kiswahili (na lugha zingine za Kiafrika) hutegemea ufadhili
kutoka kwa Wizara ya Elimu ya Marekani. Ufadhili huu huwa ni wa kushindaniwa baina ya
vyuo mabalimbali. Kila baada ya miaka minne wanaohusika hupeleka maombi yao.
Wanaokosa hulazimika kusubiri mpaka baada ya miaka minne. Vyuo vingi huona ugumu au
hukataa kuchukua masomo haya kwa sababu ya gharama, na pia baadhi ya viongozi hawaoni
faida ya masomo haya kwa Wamarekani na kwa hivyo huyapinga sana. Hata pale msaada
unapotolewa huwa hautoshi kukidhia mahitaji ya usimamizi, ufundishaji, na utengenezaji wa
vifaa vya kufundishia lugha hizi. Kuna vyuo kadha ambavyo vimejitahidi kuimarisha
programu za lugha za Kiafrika. Baadhi ya vyuo hivi ni Yale, Harvard, UCLA, Chuo kiuu cha
Indiana (Bloomington), Chuo kiuu cha Georgia (Athens), Michigan State, na Chuo kiku cha
Illinois (Urbana Champaign) miongoni mwa vingine.

4. Uhaba wa Wanafunzi 

Siku hizi mambo mengi yanafasiriwa kiuchumi. Kwa sababu ya gharama ya elimu wanafunzi
hutaka kujua faida ya kujifunza Kiswahili. Kwa vile Kiswahili hakitumiki kama lugha ya
kufundishia elimu ya juu (kama vile Kiingereza, Kifaransa, n.k), huonekana kama lugha duni
na ambayo matumizi yake si ya kimsingi katika kiwango cha taaluma za juu. Mradi katika
Afrika lugha za kigeni zimepewa kipaumbele, itaendelea kuwa vigumu kukiendeleza
Kiswahili kama lugha ya kigeni. Uhaba wa wanafunzi pia huathiri kiasi cha usaidizi
unaotolewa na vyuo. Kila mwisho wa mwaka, takwimu za idadi ya wanafunzi waliojisajilisha
madarasani huhitajika na madarasa ambayo huwa na wanafunzi wachache huwa na tisho la
kufungwa. Ni muhimu kukumbuka kuwa wanfunzi huwa na uwanja mkubwa wa kuchagua ni
lugha ipi wajifunze. Pana haja ya kubadilisha sera za lugha barani Afrika ili kuzipa lugha zetu
umuhimi zaidi. Kuzikuza huko na kuzipa hadhi ndiko kutazifanya zitambulike na kuwavutia
wanafunzi wengi.

5. Maabara 

Ingawa vyuo vingi vina maabara za kompyuta, ni vyuo vichache vilivyo na maabara
iliyotengwa kwa maksudi ya lugha za Kiafrika. Mpaka sasa ni Chuo Kikuu cha Wisconsin-
Madison na Chuo Kikuu cha Georgia vilivyo na maabara ya lugha za Kiafrika. Vyuo vingine
huwa na maabara ya lugha za kigeni na uhitaji huzidi nafasi zilizomo kwa sababu ya wingi wa
lugha za kigeni zinazofundishwa. Pia baadhi ya vyuo huwa na wakati maalum wa kufundisha
lugha za kigeni. Kwa mfano katika Chuo Kikuu cha Yale madarasa yote ya mwaka wa
kwanza ya lugha za kigeni hukutana saa tatu na nusu asubuhi Jumatatu mpaka Ijumaa. Kwa
hivyo ili kupata nafasi ya kutumia maabara ni lazima kutuma maombi mapema.

  Tatizo lingine ni uhaba wa programu za kompyuta za Kiswahili. Kwa mfano mpaka sasa
hakuna programu ya kusahihisha tahajia ya Kiswahili na uakifishaji (punctuation). Baadhi ya
vifaa  vya  kufundishia  Kiswahili  kwa  kompyuta  vilivyoko  vimetengenezwa  na
wafanyabiashara na nyingi hazifai kwa matumizi ya darasani. Hata kule kuliko na mitambo ya
kompyuta, walimu wengi bado wanahitaji mafunzo na uzoefu wa matumizi ya vifaa hivi.
Kama vile ni vigumu kwa kipofu kumwongoza kipofu mwingine njia, mwalimu asiye na
welendi wa matumizi ya kompyuta hawezi kuwafundisha wanafunzi kwa kutumia kifaa kile.


Mapendekezo ya Suluhisho kwa baadhi ya Matatitzo/Vikwamizi

Kuwa na walimu waliofuzu na wa kudumu kunaweza kusaidia kukua kwa programu kwa njia
mbalimbali. Kwanza kunaweza kuwavutia wanafunzi katika madarasa ya lugha za Kiafrika
(ya Kiswahili ikiwemo). Wanafunzi wengi wa vyuo Marekani hujua zaidi kuhusu masomo na
hasa ya lugha kupitia kwa wanafunzi wengine. Katika utafiti mdogo uliofanywa na
mwandishi wa makala hii, wanafunzi walipoulizwa jinsi walivyojua kuhusu lugha ya
Kiswahili, wengi (asilimia 60) walisema ni kupitia kwa wanafunzi wengine (Wa'Njogu 2001
na 2005). Kwa sababu ya mafunzo na ujuzi mwalimu aliyefuzu atakuwa na mbinu za
kuwavutia na kuwahamasisha wanafunzi na hivyo kuongeza idadi. Walimu waliohitimu na
wa kudumu wataipa programu sifa kutokana na kushiriki kwao katika kongamano mbalimbali
za taifa na kimataifa. Walimu hawa pia wanaweza kupelekea kushawishika kwa vyuo
kugharamia programu za lugha za Kiafrika, na hapo kuondoa kutegemea Wizara ya Elimu.

  Ingawa kuna vitabu na vifaa vichache, bado kuna haja ya kuendelea kutayarisha zaidi.
Vitabu vinavyotumiwa madarasani havitoshelezi mahitaji ya chuo, programu, walimu na
wanafunzi. Kuna haja ya kuchapisha vitabu zaidi vya marejeleo vinavyoelezea dhana na
vipengele tofauti vya lugha na utamaduni. Kitabu kilichochapishwa na NALRC (National
African Language Resource center) cha marejeo ni mwanzo mzuri lakini kina udhaifu wake.
Kamusi pia zilizoko Marekani, kwa mfano ya Awde, haziwafai sana wanafunzi kwa sababu
hazionyeshi matumizi ya maneno. Wanafunzi huvunjika moyo wanapokosa neno fulani katika
kamusi, au wakiona maneno yana maana nyingi na hawakutolewa mifano ya matumizi.
Kamusi zinazochapishwa na TUKI (Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili) zingefaa sana, lakini
mara nyingi hazifiki Marekani na zikifika huwa ghali mno. Wanafunzi walio na bahati ya
kufika Kenya au Tanzania huhiari kuzinunua huko. Kamusi ilioko kwenye mtandao (Swahili
Internet Living Dictionary), bado haijakamilika na jitihada bado zinafanywa za kutafuta
wafadhili ili mradi huo ukamilishwe.

  Kwa vile siku hizi wanafunzi wana kompyuta zao, na madarasa mengi ya kisasa yana
huduma za mtandao, itakuwa rahisi kuwahimiza wanafunzi kuzileta kompyuta zao
madarasani na kutumia. Pana haja kubwa kwa walimu wa Kiswahili kushirikiana na
wataalamu wa mitambo ya kompyuta ili wapangiwe warsha za mara kwa mara na kutolewa
mafunzo ya matumizi ya vifaa hivi.

Hitimisho

Umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika elimu ya Marekani hauwezi kudunishwa. Hata hivyo
pana haja ya kujitolea zaidi kwa viongozi wa vyuo na taasisi za elimu ya juu katika
kuzifadhili programu za lugha hii. Waalimu wa lugha ya Kiswahili (popote walipo)
wanastahili kuonyesha umuhimu wa lugha hii kwa wanafunzi wa kigeni. Tusipojitolea katika
kuikuza lugha hii na kuipa hadhi barani Afrika, itaendelea kuwa vigumu kuvishawishi vyuo
kuendelea kuifundhisha. Kuna haja ya kuwa na usawazishaji wa malengo na shabaha ya
mafunzo ya lugha hii. Mambo yalivyo sasa wanafunzi hufundishwa vitu tofauti hata wakiwa
katika viwango sawa. Tofauti hii inafanya vigumu kwa wanafunzi wanaohama kutoka chuo
kimoja hadi kingine kuendelea na programu ya Kiswahili.

  Vifaa vyenye picha na sauti, kama vile kanda za video na visahani vya CD, VCD na DVD,
hutoa nafasi na kukuza uwezo wa kufikiri na ubunifu miongoni mwa wanafunzi. Vifaa hivi
pia huonyesha mazingira katika uhalisi wake. Zaidi ya kufundishia lugha, vifaa hivi huwa njia
rahisi ya kufundishia vipengele tofauti vya utamaduni. Aidha vifaa hivi hutoa nafasi nzuri ya
mjadala katika lugha husika kutegemea fasiri za wanafunzi. Kwa hivyo pana haja ya
kuendelea kutengeneza vifaa vinavyochukua mwelekeo huu.

  Ingawa lugha ya Kiswahili si mojawapo wa lugha kuu za kigeni zinazofundishwa
Marekani, si sababu ya kubakia nyuma kitekinolojia. Wengi wa wanafunzi wanaojisajilisha
katika madarasa ya Kiswahili huwa wamejifunza lugha nyingine ya kigeni (vyuoni au katika
shule za sekondari (Wa_Nogu 2001 na 2005) na huwa wameona vifaa vya tekinolojia
vinavyotumiwa na hutarajia lugha zetu nazo ziwe zimejikakamua kwa kiasi fulani katika
uwanja huu. Pia masomo mengi sasa yanahusisha matumizi ya tekinolojia, na kwa hivyo
Kiswahili ni lazima kijiunge na mkondo huu kama kinataka kushindania wanafunzi na
masomo mengine na kushindania nafasi katika lugha kuu ulimwenguni. Ingawa lugha ya
Kiswahili (na lugha zingine za Kiafrika) inakabiliwa na shida mbalimbali, kuna uwezekano
wa kukikuza na kuwa somo linalojisimamia. Kinachohitajika ni ushirikiano mkubwa mingoni
mwa walimu na vyuo Marekani, Ulaya na katika Afrika katika jitihada za kulikuza somo hili.



Marejeleo

Awde, N. 2004. Swahili-English & English-Swahili. New York, New York: Hippocrene
     Books.

Batibo, H.M. 2003. The teaching of Kiswahili as a Foreign Language in Africa: A Case of
     Study from Eastern and Southern Africa. Journal of the African Language Teachers
     Association, 3:19-34.

Biersteker, A. and Bennett, P. 1986. On Categorizing Language Courses: Reconciling Langu-
     age Characteristics and Performance Expectations. The Design and Evaluation of Afri-
     can Language Learning Materials. Proceedings of the Spring 1984 Conference on
     Developing Guidelines for the Evaluation of African Language Learning Materials,
     East Lansing, Michigan, April 13-14, 1984, imehaririwa na D. J. Dwyer. East Lansing,
     MI: Michigan State University. (Microfiche).

Biersteker, A. (22005). Masomo ya Kisasa: Contemporary Readings in Kiswahili. Trenton,
     NJ: Africa World Press

Bokamba, E.G. 2002. African Language Program Development and Admininstration: A
     History and Guidelines for Future Programs. Madison, WI: NALRC Press.

Folarin-Schleicher, A. & L. Moshi. 2000. The Pedagogy of African Languages: An Emerging
     Field. Columbus: The National East Asian Languages Resource Centre, Ohio State

University & Madison: The National African Language Resource Centre, University
     of Wisconsin-Madison.

Gardner, R.C. 1996. Motivation and L2 Acquisition: Perspectives. Canadian Journal of Psy-
     chology, 13: 266-172.

Hinnebusch, T. & Mirza, S. 1998. Kiswahili: Msingi wa Kusoma, Kusema na Kuandika. Lan-
     ham, MD: University Press of America.

Mazrui, A. M. 1997. The Future of African languages in the American Academy. Prism, 3, 1:
     Uk. 1-3.

Moshi, L.J. 1988. Tuimarishe Kiswahili Chetu. Lanham, MD: University Press of America.

Moshi, L.J. 1998. Kiswahili Language and Culture. Kensington, MD: Dunwood.

Mugane, J.M. 1999. Tujifunze Kiswahili. Athens, OH: Aramati Digital Technologies Publica-
     tions.

Odlin, T. 1989. Language transfer: Crosslinguistic Influence in Language Learning. Cam-
     bridge, NY: Cambridge University Press.

Sanneh, S. & A. Omar. 2002. African Language Study in the 21st Century: Expansion
     through Collaboration and Technology. Unpublished paper presented at the 45th ASA
     Annual Conference, Washington, DC. December 05.08.2002.

Senkoro, F.E.M.K. 2003. Tuseme Kiswahili: A Multidimentional Approach to the Teaching
     and Learning of Swahili as a Foreign Language. Madison, WI: NALRC Press. 

Wa_Njogu, J.K. 2001. A Descriptive Study of Motivation, Ethnicity, Gender, and Achieve-
     ment in Kiswahili as a Foreign Language in a College Setting: Students' Perspectives.
     Unpublished Ph.D Dissertation, Ohio State University, Columbus.

Wa_Njogu, J.K. 2005. Motivation, Ethnicityy, and Gender versus Achievement in Kiswahili
     as a Foreign Language in a College Setting: A Correlational Study. Journal of the Af-
     rican Language Teachers Association, 6: 45-66.

Zawawi, S. 1988. Kiswahili kwa Kitendo. Trenton, NJ: Africa World Press.

Filamu

Kibira, J. 2003. Bongoland. Dar es Salaam: Kibira Films International.

Kibira, J. 2006. Tusamehe. Dar es Salaam: Kibira Films International.

Kibira, J. 2007. Bongoland II. Dar es Salaam: Kibira Films International.

Mazrui, A. The Africans: A Triple Heritage. Washington, D.C.: Annenberg/CPB Project.

Mulvihill, R. & M. Mhando. 2000. Maangamizi. Encino, CA: Gris-Gris Films.

Nangayoma, N. & Mulvihill, R. 1983. Arusi ya Mariamu. Encino, CA: Gris-Gris Films.



Kurasa za Mtandao

Mugane, J. 2007. Salama. http://www.aramati.org/ (Tarehe 2, mwezi wa Januari, 2009).

Moshi, L. & A. Omar. 2000. Kiswahili kwa Kompyuta (KIKO). African Studies Institute,
     University of Georgia, Athens. http://africa.uga.edu/Kiswahili/doe/ (Tarehe 2, mwezi
     wa Januari, 2009).

Benjamin, M. &, A. Biersteker. 1994. The Kamusi Project. http://www.kamusiproject.org/
     (Tarehe 2, mwezi wa Januari, 2009).

Visahani vya CD

The Rosetta Stone. 2007. The Rosetta Stone V2. Swahili Level 1. CD-ROM. Arlington: Ro-
     setta Stone Ltd.




                                    




Sambaza hii :

0 maoni:

Tafuta Kwenye Wikipedia

Matokeo ya utafutaji

 
Kwa Hisani ya : Muunda Blogu | Nawaje Ali | NAM
Fahari kwa Kiswahili Jukwaani
Hakimiliki © 2013 - 2018. Kiswahili Jukwaani - Haki Zote Zimehifadhiwa