Kazi Kazini…!
Mtoto wangu nampenda sana. Najitahidi kumpatia malezi bora. Nashughulishwa na chakula alacho, maarifa apatayo na tabia akuliazo. Kwa kuwa nataka awe bora, namfuatilia sana akiwa nyumbani na zaidi awapo mazingira yaliyo mbali na nyumbani. Huko hupenda kujua yuko wapi, anafanya nini, anafanya vipi, yuko na nani katika mazingira na muda gani? Namtakia mafanikio mwanangu. Nataka atengenee. Naamini kuwa mafanikio yake yanategemea sana jitihada za malezi yangu kwake. Kawaida yangu ni kutochelea kilio cha mwana. Haidhuru, wakati mwingine, mtoto akililia wembe… Si kawaida yangu kucheka na mtoto katika mazingira yasiyo ya lazima. Hofu yangu ni kama vile kucheka na nyani… Najua kuwa tabia hii ya mfumo wa malezi niitumiayo na kuikuza kwa mtoto wangu si yenye kuridhiwa kwake. Natambua shida na usumbufu wake. Naamini siku zote kuwa, …chumia juani ulie kivulini! Si kwamba huwezi kuchumia kivulini na kulia papo, lakini hii ni kama shabaha ya kunguru… Mimi ni mzazi.
Wanajamii walionizunguka wanahitaji maarifa. Nipo kwa ajili yao. Jukumu langu ni kutoa taaluma. Natambua kuwa nina dhima kubwa. Nafahamu sana kwamba hili ni jukumu zito. Hata hivyo, najitahidi kuhakikisha kwamba jamii yangu inapata ‘elimu bora’ na kamwe si ‘bora elimu’. Elimu kwa kujitegemea. Elimu kwa kujikomboa. Elimu kwa kujitambua. Napenda kuona wanafunzi wangu wanaweka kwenye matendo kila dhana mpya wajifunzayo. Mabadiliko ya kiutendaji yaonekane kwa wanafunzi wangu. Thamani ya wanafunzi wa elimu ya Sekondari isilingane na ile ya wanafunzi wa elimu ya juu (Chuo). Dhamiri yangu ni kuwajengea wanafunzi wangu uwezo wa kujithamini na kuthamini uwezo wao. Wanafunzi wangu wajali wajifunzayo na wajifunzavyo. Wathamini mambo muhimu na umuhimu wa mambo hayo. Wauthamini wakati na umuhimu wake. Watambue mabadiliko ya wakati na athari za elimu wajifunzayo katika kupambana na maisha. Ndio maana, sipendi kulinyamazia kosa loloto (kubwa au dogo) lifanywalo na (m)wanafunzi wangu mbele yangu (machoni au kulishuhudia katika mazingira mengine). Nipendalo kuliona na ninalosisitiza zaidi kwa wanafunzi wangu ni kuitumia elimu (hata iwe ya kiwango cha chini, ilimradi ni ‘elimu bora’) katika maisha ya kila siku. Mimi ni mwalimu.
Nimepewa kazi ya kusimamia usalama wa watembeao barabarani. Kuna watembeao kwa miguu, baiskeli, pikipiki, gari, n.k. Jitihada niifanyayo ni kuhakikisha kwamba kila mtumia barabara hasumbuki. Sipendi kuona, kwa mfano, gari imebebeshwa watu (abiria) zaidi ya kiwango kilichowekwa; chombo kinatembea mwendokasi zaidi ya mwendo unaopaswa kulingana na mazingira na wakati kipitao chombo; kupita sehemu au upande na mazingira yasiyostahiki; n.k. Nataka kila mtu awe salama. Ndiyo maana kazi yangu inaitwa usalama wa raia. Kwa jitihada zote, napenda kuwajibika kwa mujibu wa sheria. Huwa nasimama barabarani kwa muda ninaotakiwa na siondoki hadi muda wangu uishe. Katika kutekeleza majukumu yangu, sipendi kulifumbia macho kosa lolote (hata liwe dogo kiasi gani). Aidha, utiifu wa mtumia barabara kwa sheria au utaratibu wowote ndiyo furaha na mafanikio ya kazi yangu. Mimi ni usalama barabarani.
Nimekutana na wafanyakazi wenzangu. Mzazi, mwalimu, usalama wa taifa, n.k. Wote, kwa nyakati tofauti, kutegemea jukumu la kila mmoja, wanalalamika. Wanasema wana “kazi kazini…!”. Fikiria sifa zao, thamani yao na majina yao kwa jamii.
HAMAD, A. S.
0782197593
kiswahilikwakiswahili@yahoo.com
0 maoni:
Chapisha Maoni