Matini Muhimu :
Home » » Hila Zina Maulaya

Hila Zina Maulaya

Imeandikwa na; Unknown mnamo, Jumatano, 1 Januari 2014 | Jumatano, Januari 01, 2014




  HILA ZINA MAULAYA 

Nijapotendwa ubaya, na wabaya kiwajua, 
Mwenzao huona haya, ubaya kuwatendea, 
Japo moyo una maya, hufanya kuuzuia, 
Nacheka hali najua, hila zina Maulaya. 

Hila zina Maulaya, Nacheka kumbe najua, 
Za watu hila kayaya, mwisho utu zawatoa, 
Haki iwapo sawiya, Mola atanitetea, 
Wangawa zana watia, hila zina Maulaya. 

Hila zina Maulaya, wangawa zana watia, 
Sina kosa sitapwaya, Mola tanisaidia, 
Japo animeze chweya, pwani tanitapikia, 
Na wakinishambulia, hila zina Maulaya 

Hila zina Maulaya, na wakinishambulia, 
Nyama ilooza mbaya, mbesi huifurahia, 
Simba huona vibaya, kula kilojiozea, 
Japo zoga la ngamia, hila zina Maulaya 

Hila zina Maulaya, japo zoga la ngamia, 
Mbesi wanachekelea, simba aona udhia, 
Zoga likijiishia, na mafupa kusalia, 
Ndipo watalikimbia, hila zina Maulaya. 

Hila zina Maulaya, beti sita twaishia,  
Kaluta kanena haya, zamaze zimemwishia, 
Sasa mekuwa hekaya, kutenda kwa mazoea, 
Zama zilizosalia, hila zina Maulaya. 



{Chanzo: Kaluta Amri Abedi, 1953:63-64} 
*Beti ya mwisho tumeiongeza sisi. 
  
Tuma maoni yako kwa: 
                                                  HAMAD, A. S. 
                                                  0782 197 593 
                                                  kiswahilikwakiswahili@yahoo.com 
Sambaza hii :

Tafuta Kwenye Wikipedia

Matokeo ya utafutaji

 
Kwa Hisani ya : Muunda Blogu | Nawaje Ali | NAM
Fahari kwa Kiswahili Jukwaani
Hakimiliki © 2013 - 2018. Kiswahili Jukwaani - Haki Zote Zimehifadhiwa