HILA ZINA MAULAYA
Nijapotendwa ubaya, na wabaya kiwajua,
Mwenzao huona haya, ubaya kuwatendea,
Japo moyo una maya, hufanya kuuzuia,
Nacheka hali najua, hila zina Maulaya.
Hila zina Maulaya, Nacheka kumbe najua,
Za watu hila kayaya, mwisho utu zawatoa,
Haki iwapo sawiya, Mola atanitetea,
Wangawa zana watia, hila zina Maulaya.
Hila zina Maulaya, wangawa zana watia,
Sina kosa sitapwaya, Mola tanisaidia,
Japo animeze chweya, pwani tanitapikia,
Na wakinishambulia, hila zina Maulaya
Hila zina Maulaya, na wakinishambulia,
Nyama ilooza mbaya, mbesi huifurahia,
Simba huona vibaya, kula kilojiozea,
Japo zoga la ngamia, hila zina Maulaya
Hila zina Maulaya, japo zoga la ngamia,
Mbesi wanachekelea, simba aona udhia,
Zoga likijiishia, na mafupa kusalia,
Ndipo watalikimbia, hila zina Maulaya.
Hila zina Maulaya, beti sita twaishia,
Kaluta kanena haya, zamaze zimemwishia,
Sasa mekuwa hekaya, kutenda kwa mazoea,
Zama zilizosalia, hila zina Maulaya.
{Chanzo: Kaluta Amri Abedi, 1953:63-64}
*Beti ya mwisho tumeiongeza sisi.
Tuma maoni yako kwa:
HAMAD, A. S.
0782 197 593
kiswahilikwakiswahili@yahoo.com
1 maoni:
Limekaa sawia.
Chapisha Maoni